UKIMUULIZA shabiki yeyote wa soka duniani, atakwambia kwa sasa
kuna mwamuzi mmoja tu maarufu, Howard Webb.Sifa yake ni kuchezesha mechi
ya fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania na Uholanzi nchini Afrika
Kusini mwaka 2010.
Pia hata mechi ngumu za Ligi Kuu England au Ligi
ya Mabingwa Ulaya amekuwa akipangwa kuchezesha. Sahau hilo la Webb.
Tanzania kuna mtu mmoja anaitwa Kipunje.
Huyu jamaa anaishi sehemu moja inaitwa Mwananyamala B, Mtaa wa Ujiji, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Unaweza ukashangaa, lakini huyo Kipunje ndiyo
mwamuzi ghali zaidi wa mechi za mchangani kwenye wilaya zote tatu za Dar
es Salaam ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni.
Ndiye mwamuzi pekee anayeweza kufanya kitu ambacho hata Webb au mwamuzi yeyote wa Fifa hawezi kuthubutu kukifanya.
Ndiye mwamuzi wa Dar es Salaam, ambaye ni maarufu
zaidi katika mechi za mchangani na anayechezesha mechi yoyote
iliyoshindikana kutokana na vurugu za mashabiki au wachezaji, haogopi
chochote ndiyo maana thamani yake ipo juu tofauti na wengine.
Ukikutana naye ana kwa ana mtaani huwezi kuamini
kwamba ndiye Kipunje anayeogopwa na wakorofi walioshindikana katika
Wilaya ya Kinondoni.
Unajua kwa nini anaogopwa? Ni hivi, anachezesha
mechi akiwa ametinga na silaha za jadi kiunoni ndani ya bukta yake.
Silaha hizo ni panga refu upande wa kushoto na shoka dogo upande wa
kulia.
Nani atamsogelea?
Anavyojiandaa
Anavaa jezi zake bukta, fulana, soksi na raba
kisha anafunga kamba ya katani kiunoni halafu anachomeka panga kushoto
kwake na shoka kulia.
Anachukua kadi zake ile ya njano anaweka mfuko wa
kushoto kifuani kwenye fulana yake na ile nyekundu anaichomeka kulia
ananyoosha viungo anaingia kazini.
Kivutio chake kikubwa ni silaha anazotinga na kujiamini ambako
kumefanya timu zote korofi hata wahuni na mateja wanaoingia viwanjani
kuogopa kumfanyia fujo kama wanavyofanyia waamuzi wengine.
Ndiye mwamuzi ghali zaidi. Kwa mechi moja hulipwa
kuanzia Sh20,000 hadi Sh50,000 kulingana na ugumu na mazingira hatarishi
kwenye mchezo husika.
Waamuzi wengine hulipwa kati ya Sh10,000 mpaka
Sh12,000 kwenye mechi hizo. Kama ukiwa na kiasi hicho huwezi kuzungumza
na Kipunje kwani ni ndogo mno kwake.
Mwamuzi huyo ambaye jina lake halisi ni Issa Salum Mchinjakuku.
‘Kipunje’, anasema Mchinjakuku ni jina la babu yake mzaa baba na ni mwenyeji wa Pwani.
Kwa nini anaitwa Kipunje?
“Niliitwa hilo jina kwa vile tangu nikiwa mdogo
nilikuwa napenda sana ubwabwa wa kwenye hitma, huko pia pamenifanya
kujulikana sana. Hata nikiwa na washikaji zangu tunashtuana ni wapi
kwenye ubwabwa tuibuke. Pitapita zetu kwenye hiyo minuso zimenifanya
nijulikane sana. Popote pale nakwenda ilimradi kuwe na ubwabwa.”
Chanzo cha kutumia silaha
Kipunje ambaye alizaliwa mwaka 1980 Mwananyamala
jijini Dar es Salaam, anasema alianza kufanya hivyo mwaka 2005 baada ya
kumshuhudia mwamuzi mwenzake aliyemtaja kwa jina la Wema akipigwa na
mashabiki mpaka kuzirai.
“Tukio hilo lilitokea katika Uwanja wa CCM
Mwinyijuma, Dar es Salaam ambako mashabiki wa timu ya Amstadam ya
Tandale walimdunda Wema hadi akazimia, walifanya hivyo baada ya mwamuzi
huyo kukubali bao la Mchangani FC ya Mwananyamala ambalo halikuwa na
utata wowote.
“Niliumia sana kuona mwenzangu anapigwa hivyo bila
ya kupata msaada wowote, tena ilikuwa karibu kabisa na kituo cha
polisi, lakini alidundwa vibaya na hata Polisi walipoambiwa hawakutokea
kumuokoa kwa sababu wanaujua mtiti wa wahuni wa Tandale,” anasema
Kipunje ambaye anajitambulisha kuwa ni Mzaramo.
“Hali hiyo ndiyo iliyonifanya nipate akili ya
kuingia uwanjani nikiwa na silaha, lengo likiwa ni kujilinda ili na mimi
siku moja yasije kunikuta kama yaliyomkuta mwenzangu na kama unavyoona
hakuna mhuni au mchezaji yeyote mkorofi anathubutu kunipiga iwe
amekubaliana na matokeo au anapinga wanaishia kupiga kelele tu, lakini
mimi nipo salama,” anasema Kipunje ambaye alianza kazi ya uamuzi wa soka
mwaka 2000.
“Mwaka jana silaha hizi zilinisaidia na pengine kama nisingekuwa
nazo siku hiyo ningekuwa sipo duniani sasa, ningekuwa marehemu, ilikuwa
katika Uwanja wa CCM Mwinyijuma nilipokuwa nachezesha mechi ya nusu
fainali kati ya Shideo na Baula.
“Mashabiki wa Shideo waliingia uwanjani kwa lengo
la kunipiga kwa sababu tu nilikubali bao walilofunga Baula, jamaa
walikuwa wamefura ile mbaya, niliwaacha wanisogelee kwani walikuwa
hawajui kama nina vifaa vya kazi kiunoni.
“Walipofika na kuanza kunisukuma nilichomoa panga
na wakashituka wakatoka nduki, hali iliyonipa ujasiri na mimi nikaanza
kuwafukuza, lakini bahati mbaya panga liliniponyoka na kudondoka mbali
kidogo na mimi.
“Mmoja kati ya mashabiki hao aliliwahi na
kulichukua lakini kabla hawajakaa sawa nilichomoa shoka langu na kuanza
kuwafuata kwa kasi ya ajabu, baada ya kuona hivyo jamaa alilitupa panga
hilo na kutimua mbio kama vile wamemuona mtoa roho,” anasema mwamuzi
huyo mwenye elimu ya msingi.
“Baada ya kuhakikisha wamefika mbali nilirudi
uwanjani na kuendelea na kazi yangu na hakuna mtu yeyote aliyeleta tena
chokochoko hadi mechi hiyo ilipomalizika. Kitendo hicho kilizidi
kuniongezea umaarufu katika mitaa ya Mwananyamala, Kinondoni, Tandale na
sehemu nyingine za Jiji la Dar es Salaam ambako mechi zote
zinazohusisha timu zenye mashabiki wahuni, ninakodishwa nikachezeshe
hakuna mtu yeyote anayeniletea upuuzi, nikitoa uamuzi hakuna anayebisha
kama akipiga kelele ni huko huko nje ya uwanja.
“Mbali na mashabiki pia hata wachezaji na hata
mateja ambao hukusanyika viwanjani nao wananifahamu sana na kuniogopa,
tangu wajue nina silaha nikimwonyesha mchezaji kadi nyekundu hutoka nje
kwa roho safi kabisa bila ya kunung’unika kwa sababu anajua akiniletea
ujinga atakiona cha mtema kuni.
“Hizi silaha zimenifanya niwe mwamuzi wa bei mbaya kuliko wote Wilaya ya Kinondoni.”
Familia yake inamchukuliaje
Kipunje ni baba wa watoto watatu; Zainabu (5),
Zulfa (2) na Nasra (1) na ni mume wa wake wawili anaoishi nao pamoja
nyumbani kwake Mwananyamala.
Anasema kuwa familia yake haijui kama huchezesha
soka akiwa na silaha hizo za jadi kwani anapotoka nyumbani kwenda kazini
huzificha kwenye begi maalumu lenye jezi na vifaa vingine vya uamuzi.
“Wake zangu wote wananihesimu sana na hawajui
chochote juu ya jambo hilo na hawajawahi kuniuliza, mara nyingi
ninapokuwa naondoka nyumbani nahakikisha hizo silaha hawazioni, nafanya
hivyo ili wasipatwe na wasiwasi waniogope, hiyo inaweza kusababisha
mapenzi yetu yakayumba pia sipendi watoto wangu waone,”anasema mwamuzi
huyo, ambaye ana kadi na jezi maalumu kwa mechi za mchangani na zile
zinazoandaliwa na Chama cha Soka cha Kinondoni (Kifa).
Changamoto na malengo
Anasema viongozi wa Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (Kifa)
wamekuwa wakimuonya na kumtaka aachane na silaha hizo, lakini yeye
amekuwa akigoma kwa vile ndiyo usalama wake anapokuwa uwanjani kwani
mchangani hakuna usalama na ndiko anakopatia fedha nyingi za mkupuo.
Anasema pia staili yake ndiyo imepandisha thamani yake na endapo ataiacha ataporomoka na kupotea kwa vile atakuwa hana jipya.
“Siwezi kuacha silaha zangu iwe katika mechi za
Kifa au zile za mchangani ambazo huandaliwa na watu wa kawaida, nitakuwa
nahatarisha maisha yangu kwa sababu huko mashabiki hawafai hata kidogo
wengi wanafuata fujo si mpira.
Nimewaambia nitaachana na silaha nitakapofanikiwa
kuwa mwamuzi wa Ligi Kuu Bara,” anasema Kipunje ambaye anadai ni mwamuzi
wa Kifa baada ya kufanya vizuri kwenye mafunzo ya mwaka jana.
Lakini, Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi Wilaya ya
Kinondoni, Hussein Kalindo anasema: “Bado hajawa mwanachama wetu, ila
alipata mafunzo na bado majibu yake ya mtihani hayajatoka.”
Malengo ya Kipunje
“Mungu akipenda mwezi Desemba nitahudhuria mafunzo ya TFF kujaribu bahati yangu ya kuchezesha Ligi Kuu.
Nikifanikiwa kupata nafasi hiyo naamini kuwa
heshima yangu itaongezeka pia nitaheshimu zaidi sheria 17 za soka na
nitakuwa bora zaidi kama yule mwamuzi Hashim Abdallah aliyechezesha
mechi ya Ligi Kuu ambayo Simba iliitandika Yanga mabao 5-0 au Pierluigi
Collina yule Mitaliano ambaye amewahi kuwa mwamuzi bora wa Fifa,”
anasema.
Kazi nyingine anayofanya
Ukiachana na uamuzi wa soka, Kipunje pia ni
kondakta wa daladala inayofanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka
Makumbusho kwenda Kivukoni jijini Dar es Salaam.
“Kazi hii ya ukondakta naiheshimu sana kwani ndiyo
inayonisaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha maisha yangu ya kila siku na
kuifanya familia yangu iwe na amani wakati wote japo kuna changamoto
nyingi ambazo nakutana nazo,” anasema.
BY:
Mwanaspot
BY:
Mwanaspot
0 your comments:
Post a Comment