Waandishi wawili wa habari nchini Nigeria
wamekamatwa kwa mauaji ya wahudumu tisa wa afya waliokuwa wanatoa chanjo
dhidi ya Polio mjini Kano, Kaskazini mwa nchi.
Kwa mujibu wa afisaa mkuu wa polisi, Ibrahim Idris, waandishi hao, watashtakiwa kwa kosa la mauaji.Inadaiwa waliwachochea wananchi kupitia kwenye redio kupinga chanjo hizo.
Baadhi ya viongozi wa kiisilamu Kaskazini mwa Naigeria wanaamini kuwa chanjo dhidi ya Polio huwazuia wanawake kuweza kuzaa.
Wanaiona kama njama ya nchi za Magharibi kupunguza idadi ya waumini wa kiisilamu duniani.
Upinzani kama huu ndio moja ya sababu ambazo zimesababisha Nigeria kuwa moja ya nchi tatu ambako Polio bado ni janga kubwa.
Kulingana na mpango wa kuangamiza Polio duniani, mwaka jana watu 121 waliugua Polio ikilnganishwa na waathiriwa 58 nchini Pakistan na 37 nchini Afghanistan.
Hadi sasa hakuna kundi lolote limedai kuhusika na mauaji hayo yaliyotokea siku ya Ijumaa wiki jana.
Baadhi wamewatuhumu wapiganaji wa kiisilamu wa Boko Haram kwa kufanya mauaji hayo,lakini kundi hilo bado halijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo.
Polio ni ugonjwa wa kuambukizana na unasababishwa na virusi ambavyo huvamia neva za mwili, na kusababisha ulemavu.
Unaweza kutokea katika umri wowote ule lakini hasa hasa huwaathiri watoto walio chini ya umri wa miaka 5.
0 your comments:
Post a Comment