Penye nia pana njia na mtafutaji makini huwa hachoki, ndivyo anavyosema mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dk Wayne Dyer wa Marekani katika kitabu chake cha ufanye nini kupata unachokiazimia.Licha ya kauli hii ya Dk Dyneer, kuna vijana wengi nchini wanaonekana wamekata tamaa; Wengine hufikiri kwamba kama umezaliwa katika familia duni, maana yake utakuwa na maisha duni milele, huku wale ambao wamezaliwa katika familia tajiri, wanafikiri wataendelea kuwa tajiri.
Hata hivyo ukweli ni kwamba mtu yeyote anaweza kuwa na maisha bora,
kama anavyosema msomi Hope Clark katika kitabu chake Fedha za Waandishi
cha hivi karibuni nchini Ireland, kwamba siri ya kufanikiwa katika
maisha ni kuishi kwa malengo, kuishi vizuri na watu na kupenda kuwa
karibu na wasiokata tamaa.
Mwalimu Julius Nyerere wakati fulani amewahi kunukuliwa akisema
‘Uchumi mnao, mmeukalia’. Kila mtu alitafsiri alivyoweza, lakini ukweli
hasa ni kwamba mtu yeyote akijipanga vizuri kwa maana ya kutuliza akili
yake, kukaa na watu wa kumshauri vizuri na kufanyia kazi mambo au
mipango anayoipanga, anaweza kufanikiwa anachotaka…Ni ukweli kuwa kuna
wengi wana maisha duni kwa sababu pamoja na mambo mengine ya tabia zao
za kukata tamaa, waoga wa kuthubutu.
Wengi wanasubiri wengine, wanalalamikia wengine zaidi
Mwalimu alisisitiza, nitamnukuu; “Hatuwezi kusubiri hadi watoto wetu
walio shuleni wamalize elimu yao ndipo tupate maendeleo ya kiuchumi na
kijamii.”.Kwa hali yoyote ambayo mtu inamsumbua katika maisha yake ni vizuri
kuangalia namna ya kujitegemea, badala ya kulalamikia wengine, anasema
mshauri maarufu Marekani, David Kudler katika chapisho lake alilolipa
jina Namna ya Kufanikiwa katika maisha.
Huu ndiyo ukweli wenyewe
Vijana wengi hapa nchini wamekuwa wakitamani sana kufikia mafanikio
lakini wengi wanalalamikia kuwa wanakabiliwa na changamoto ya
kukosekana kwa mbinu sahihi za kuwafikisha kwenye kilele cha mafanikio
wanayotaka. Wachambuzi wa masuala ya uchumi akiwemo Profesa Muhammad
Yunus ambaye anasifika kwa kuinua maendeleo kwa watu wa hali ya chini
Bangladesh, wanasema ili kufikia mafanikio ni lazima uchukue hatua kwa
nafasi uliyonayo, bila kujali ikoje, hii itakusaidia kupata chachu ya
kuongeza kasi ya kutekeleza hatua moja baada ya nyingine katika safari
yako.
Kuna wengi wamekuwa wakiwaza makubwa, lakini wanaishia kuona tu
wengine wakipaa. Hata hivyo ni wazi kwamba ushindi huja baada ya kufanya
harakati za kuutaka huo ushindi, siyo kukaa tu na kulalamika kama
wafanyavyo baadhi ya watu.Kati ya vijana ambao wanaonekana kupambana hadi kuweza kujenga majina
na heshima zao Duniani ni Salim Kikeke; Ni mtu ambaye kama angekata
tamaa hakika asingefika aliko sasa.
Sasa amekuwa ni mtu wa kujadiliwa na umaarufu wake hauko tu Tanzania,
bali maeneo mengi ya Dunia hasa kunakozungumzwa Kiswahili. Huyu mtu ni
kati ya watangazaji wakongwe na kivutio cha watu wengi kutoka barani
Afrika na duniani kote, lakini katokea wapi?.Salim ni Mtanzania anayetangaza vipindi mbalimbali katika Shirika la
Habari la Uingereza (BBC). Safari ya kufikia mafanikio hayo ilikuwa na
milima na mabonde, tabu na karaha.
Baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika Chuo cha Kilimo
Nyegezi, Mwanza, alikutana na changamoto kadhaa hasa ya kukosa ajira kwa
kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo. ”Nilimaliza Stashahada yangu mwaka 1994 kozi ya Umwagiliaji, kwa sasa labda ningekuwa bwana shamba au mfanyakazi wa kilimo,” anasema Kikeke.
Baada ya kumaliza chuo, juhudi za kusaka ajira zilikuwa ngumu.Kwa karibu mwaka mzima wa 1995, alikwenda katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani Arusha. “Hakukuwa na ajira na kishawishi cha kujiingiza katika uhalifu kilikuwa kikubwa,” anasema bila kueleza zaidi.Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo aliamua kuwa ‘Mwanaapolo’ kama wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite yaani kutumika kuingia kwenye mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine migodini. Baada ya kushauriwa na mama yake kuondoka mchimboni, alirejea Dar es Salaam.
Katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa akishinda kijiweni mitaa ya Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake, Joseph Mboya ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Mboya ndiye mmoja kati ya rafiki zangu ambao tulibadilishana mawazo, tulifarijiana na kufikiria matarajio ya ndoto zetu, mambo yalikuwa magumu mpaka nikafikia hatua ya kusema basi imetosha,” anasema Kikeke.
Kuingia utangazaji.
Mara baada ya kuona matumaini yakififia kupitia taaluma yake ya kilimo, Kikeke aliamua kubadilisha ukurasa wa maisha baada ya kupiga hodi katika ofisi za kituo cha TV cha CTN ambacho kilikuwa na redio wakati huo ikijulikana kama Classic FM ambayo kwa sasa ni Magic FM.
Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua uamuzi huo, haikutokea kama ajali, bali ilitokana na ushawishi aliokuwa ameupata kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa.
“Mama yangu alikuwa wa kwanza kunijengea uwezo wa kuingia katika utangazaji, alikuwa anapenda sana kusikiliza habari za redioni na alinishawishi kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea duniani, nikawa na uwezo wa kutamka maneno vizuri na kusoma habari,” anasema Kikeke.
Ilikuwa ni mwishoni mwa 1997, Kikeke alifika katika ofisi za kituo cha kurusha matangazo cha CTN. “Kwa sasa wanaita Magic FM, walikuwa wanafungua kituo kipya cha Classic FM hivyo niliomba kufanya kazi bure, nikapewa kipindi cha kucheza miziki ya Kiingereza,” anasema Kikeke
Jambo la kujifunza
Jambo la kujifunza hapa ni kwamba wakati mwingine katika kusaka ajira, kubali kufanya kazi bila ya malipo, onyesha jitihada zako, huenda ikawa ni njia nzuri ya kuajiriwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo yale ambayo huenda mtu amekwenda kwa ajili ya masomo kwa vitendo. Njia sahihi ya kukaa katika ajira usiyo na ujuzi nayo
Anasema baada ya kupata uhakika wa kuendelea na kazi hiyo, Januari mwaka 1998, Kikeke aliamua kwenda kusoma kozi fupi ya Utangazaji habari katika chuo cha uandishi wa habari cha ‘Tanzania School of Journalism (TSJ)’.
”Pale nilisoma cheti kwa miezi mitatu na kurudi tena kazini, nikaanza kusoma habari za kiingereza na Kiswahili wakati mwingine nilikuwa naenda kutafuta habari,” anasema Kikeke.
Mafanikio yameanza kuja, lakini ghafla anafukuzwa kazi!
“Hata hivyo mwezi mmoja baadaye wakanifukuza kazi kwa sababu ambazo nisingependa kufafanua zaidi,” anasema.
Wakati mwingine hata baya lina uzuri wake
Kikeke baada ya kufukuzwa kazi, hakuishia kulia mtaani, badala yake alianzisha mkakati wa kusaka ajira tena kwenye taasisi yenye hadhi ya juu zaidi, Radio Tanzania (RTD) ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1998.
”Kwa kipindi hicho Abdul Ngarawa alikuwa mkurugenzi wa RTD, nikapelekwa idhaa ya Kiingereza, ‘English Service’, na kuandaa vipindi vya muziki kila siku kuanzia saa 12:00 jioni mpaka saa 6:00 usiku,” anasema Kikeke na kufafanua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa muda ‘part-time.
Alianza kupangiwa vipindi vya kutangaza baada ya kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja. “Baadaye nikapewa kipindi cha Mwelekeo kilichoanzishwa wakati wa maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, nilikuwa mtangazaji wa mwanzoni kabisa katika kipindi hicho,” anasema Kikeke.
Katika kipindi hicho, Radio Tanzania walianzisha kituo cha matangazo cha FM, kiitwacho PRT kikitoa matangazo kwa lugha ya Kiingereza.RTD na Kituo cha PRT ndizo kwa sasa zinafahamika kama TBC na TBC1. “Mimi nikaondoka pale na kurudi tena CTN,” anasema.
Kurudi CTN
Baada ya kurudi katika kituo hicho, Kikeke alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma habari kwenye TV mpaka mwezi Agosti wakati kampuni hiyo ilipouzwa na kuwa chini ya kituo cha Channel Ten na DTV. Baadae alihamia ITV.
Kuingia ITV/Radio One
Baada ya hapo alifanikiwa kuandika barua ya maombi ya kazi katika Kituo cha Radio One.
“Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Radio One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya kipindi chochote nilichowahi kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila nikawa na ya TV”, anasema Kikeke.
Anaongeza kuwa hali hiyo ikamfanya abadilishe mlango wa kutoka Redio One na kuingia ITV. “Charles Hilary akaipeleka ile demo upande wa televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na Joyce Mhaville, wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,” anasema.
Kikeke alipangiwa jukumu la utangazaji wa vipindi vya taarifa za habari kila siku na habari za ‘Jiji Letu’ hata hivyo mambo yalibadilika kwa muda mfupi pale ofisini.
Safari ya BBC,
Radio One walikuwa ni Redio washirika wa BBC hivyo walikuwa na mkataba wa kuchukua mtangazaji mmoja kila mwaka na kumpeleka kufanya kazi makao makuu ya BBC kwa muda wa miezi kadhaa.
Anasema Mwezi Mei 2003 nikafaulu majaribio ya kuingia BBC, ambako anaendelea hadi leo.
Familia yake
Kikeke ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu. Ni baba wa mtoto mmoja ambaye anasoma darasa la saba nchini. “Huku London ninaishi peke yangu,” anasema.
Source:Mwananchi.
0 your comments:
Post a Comment